Rais Magufuli asema hatochoka kubadili mawaziri

Rais Magufuli asema hatochoka kubadili mawaziri

MagufuliHaki miliki ya pichaIKULU
Rais wa Tanzania John Pombe Magfuli amesema hatachoka kufanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri kila itakapohitajika.
Ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake, tayari Magufuli ameshafukuza kazi mawaziri tisa kati ya 19 aliowateua Desemba 10, 2015.
Akizungumza leo Ikulu katika hafla ya kuwaapisha mawaziri wapya, Rais Magufuli amesema ataendelea kufanya mabadiliko ya baraza lae pale patakapokuwa na uhitaji wa kufanya hivyo.
"…hii ni kama safari, sio lazima wote tufike. Inawezekana hata mie kiongozi nisisfike lakini lengo letu lazima litimie," amesema Magufuli.
Mawaziri wapya walioapishwa leo ni Japhet Hasunga kuwa Waziri wa Kilimo na Joseph Kakunda kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Ambao wametimuliwa katika nafasi hizo ni Dkt. Charles Tizeba na Charles Mwijage mtawalia.
Mawaziri hao wawili wamekuwa wahanga wa sakata la korosho lakini kwamujibu wa Magufuli utendaji wao wa kazi ulikuwa unamkwaza siku nyingi.
Magufuli, Majaliwa, TizebaHaki miliki ya pichaIKULU
Image captionCharles Tizeba (kushoto) ametimuliwa katika nafasi yake ya uwaziri wa kilimo.
Magufuli 'alipovamia' mkutano kati ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na wanunuzi wa sekta binafsi tarehe 28 Septemba aligundua 'madudu' mengi ambayo yangeweza kutatuliwa na wizara hizo mbili na bodi ya korosho lakini hawakufanya hivyo mapema.
"Kwenye mkutano ule nilikuta bodi ya korosho imetoa bei elekezi ya Sh1,500, iliniumiza sana...lakini mwisho wa yote unajiuliza wizara ya kilimo ipo wapi? Au Mwijage nae alikuwa tu na viwanda akasahau wafanyabiashara ya korosho."
Katika mkutano wa Oktoba 28, Magufuli na wafanyabiashara walikubaliana bei elekezi ya Sh3,000 lakini utekelezaji wake ulisuasua. "Sikuona tamko lolote kutoka kwa Waziri wa Kilimo au Biashara kukemea kile ambacho kilikuwa kinaendelea, mpaka ikabidi nimtume Waziri Mkuu awape wanunuzi siku nne tu wafanye maamuzi."
'Kila Kitu Waziri Mkuu'
Magufuli pia ameiambia hadhara iliyokuwepo ikulu kuwa alishawahi kumwambia Waziri Mkuu kuwa atamfanya kuwa Waziri wa Kilimo kutokana na kutatua changamoto nyingi za wiazara hiyo.
"Kulipokuwa na shida ya bei ya kahawa mkoani Kagera, ilibidi Waziri Mkuu aende akalimaliza ndani ya moda mfupi. Sasa najiuliza Mwijage hakuliona hili na yupo karibu, lakini kahawa nizao la kilimo hawakuchua hatua pia."
Magufuli na MajaliwaHaki miliki ya pichaIKULU
Image captionRais Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa walipokutana na wanunuzi wa korosho Oktoba 28
Waziri Majaliwa alienda Kagera mwezi Oktoba na kutangaza mfumo mpya wa minanda ya kahawa na kumaliza sakata hilo.
Changamoto nyengine ilikuwa ya kiwanda cha chai cha Mponde Tanga ambacho kilikuwa hakifanyi kazi kwa zaidi ya miaka mitano lakini Majaliwa akamaliza mgogoro wake mapema mwezi huu.
"Sio kama siwapendi, nampenda Tizeba nataniana na Mwijage lakini katika hili nimeona siwezi tena kuwasukuma, nitawavunja miguu. Wacha hawa wapya waje waendane na spidi."
Mawaziri Waliotoswa
Mwezi Mei 2016, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Charles Kitwanga alifutwa kazi kwa tuhuma za kuingia Bungeni akiwa amelewa.
Mawaziri wawili Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini) George Simbachawene (Ofisi ya Rais) walifutwa kazi kufuatia sakata la mchanga wa madini (makinikia) wa kampuni ya Acacia.
Julai mosi mwaka huu Mwigulu Nchemba alitolewa kwenye nafasi ya uwaziri wa Mambo ya Ndani. Rais Magufuli alitaja sababu 13 kumwondoa Mwigulu ikiwemo ajali za barabarani na matumizi mabaya ya fedha za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.
Mwezi Machi 2017 Nape Nnauye aliyekuwa Waziri wa Habari alitimuliwa kazi. Mkuu wa Mko wa Dar es Salaam, Paul Makonda alivamia Kituo cha Televisheni cha Clouds akiwa na askari wenye silaha akitaka kipindi anachotaka yeye kirushwe hewani.
Nape akiwa kama waziri mwenye dhamana, akaitisha uchunguzi huru wa tukio hilo. Ripoti ya uchunguzi huo ilimtia lawani Makonda.
Nape aliahidi kuifikisha ripoti hiyo kwa Rais, lakini hatimaye alifutwa kazi, na badala yake Magufuli, mbele ya hadhara akamsihi Makonda " piga kazi" na kusema yeye Rais hapangiwi nini cha kufanya.
Mawaziri wengine waliotimuliwa kazi ni Prof Jumanne Maghembe (Maliasili na Utalii) na Gerson Lwenge (Maji na Umwagiliaji).

Comments

Popular posts from this blog